MAALIM SEIF AHIMIZA VIONGOZI KUPUNGUZA UMASIKINI
Makamu wa kwanza wa Rais wa
Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad amesema Tanzania inakabiliwa na changamoto
kubwa za kutokomeza umasikini kutokana na baadhi ya viongozi wa serikali
kuendekeza ufisadi wenye maslahi binafsi badala ya wananchi.
Ametoa kauli hiyo wakati
akiweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za makao makuu ya Chama Cha
Wananchi-CUF Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF anatoa
kauli hiyo ikiwa ni siku chache tu baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kufuatia
baadhi wa mawaziri kuhusishwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma.
Amesema licha ya Tanzania kuwa na rasilimali za
kutosha lakini bado wananchi wake hawanufaiki nazo kutokana na tamaa ya baadhi
ya viongozi wake.
Amesema wakati nchi ikiwa imetimiza miaka 50 ya uhuru bado
suala la ufisadi limekuwa changamoto kubwa hali inayodidimiza uchumi wa Taifa
na kusababisha Mfumuko wa bei za bidhaa kwa watanzania.
Ujenzi wa ofisi hizo unakadiriwa kutumia Sh milioni 13
tu mpaka kukamilika kwake ambapo Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara
Julius Mtatiro anasema hatua hiyo ya uzenzi wa gharama nafuu unaonyesha jinsi
chama hicho kinavyopingana na ufisadi.
Akisoma Taarifa ya ujenzi wa ofisi hiyo Kaimu Katibu
wa CUF Wilaya ya Kinondoni Kassim Hamis
amesema hadi sasa zimekwisha tumika Sh milioni tatu na sabini na sita elfu
licha ya juhudi hizo kufanyika lakini kumekuwepo na makundi ndani ya chama
hicho yanakwamisha maendeleo.
Suala la ufisadi,uwajibikaji na utawala bora limekuwa
likijadiliwa sana katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni na hasa tangu baada
ya kuibuka kwa kashfa ya Richmond hadi sasa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment